Tunafanya nini

Sehemu kuu za Programu ya FORVAC

FORVAC inakusudia kuongeza faida za kiuchumi, kijamii na kimazingira kutokana na misitu kwenye eneo la programu kupitia utekelezaji wa sehemu kuu nne kama ifuatavyo:
Uanzishaji na uhamasishaji wa Hifadhi za misitu ya vijiji (VLFRs) ni sehemu ya kwanza katika maendeleo ya mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu. Mipango ya matumizi bora ya ardhi ni hatua muhimu katika kuhakikisha umiliki wa kudumu na usimamizi endelevu wa hifadhi za misitu ya vijiji.

Misitu ya vijiji ipo katika hatua mbalimbali za maendeleo, mingine imedhinishwa katika ngazi ya wilaya kwa kuidhinishiwa mipango ya usimamizi wa misitu pamoja na sheria ndogo ndogo. Aidha, misitu mingine imekamilisha sehemu tu ya hatua zinazohitajika katika uanzishwaji, mfano; vijiji vingine havina Mipango bora ya matumizi wa ardhi. FORVAC inafanya kazi ya kuandaa na kurejea hatua za uandaji wa mipango ya usimamizi wa misitu ya vijiji.

Jamii na ushiriki wa sekta binafsi

Mbali na uanzishwaji na uhamasishaji wa Hifadhi za Misitu ya Vijiji, jamii zinahitaji uwezeshwaji kwa maendeleo ya minyororo ya thamani wa mazao ya misitu ambayo iko chini ya Usimamizi wa jamii na vijiji. FORVAC itasaidia vikundi vya wazalishaji ndani ya vijiji husika na pia ushiriki wa sekta binafsi katika ngazi yoyote ya mnyororo wa thamani.

Jukumu la sekta binafsi ni muhimu katika Programu. Mbali na jamii, mashirika ya sekta binafsi, haswa wajasiriamali wanaojishughulisha na uvunaji wa bidhaa za misitu, usindikaji, usafirishaji na uuzaji wana jukumu muhimu katika utekelezaji wa programu hii. Kampuni binafsi na taasisi zisizo za kiserikali zinajihusisha na utekelezaji wa Programu chini ya mikataba ya utoaji wa Huduma au kama watendaji au wadau katika mnyororo wa thamani. Kampuni binafsi na wafanyabiashara wa ndani, kwa mfano, viwanda vya kupasua mbao, wapasua mbao wadogo, wafanyabiashara wa mkaa, kampuni za usindikaji asali na kampuni ya masoko ni miongoni mwa wanufaika wa programu hii kupitia ushiriki wao katika kuendeleza minyororo ya thamani ya mazao ya misitu.

Vijiji vyote vinavyolengwa vinahitaji kujengewa uwezo na ujuzi katika kusimamia hifadhi ya misitu ya vijiji (VLFRs) na maendeleo ya mnyororo wa thamani ndani ya jamii, pia ikihusisha vikundi vya wazalishaji. Wanavijiji na wanachama wa Kamati za maliasili za viijiji na halmashauri za vijiji zinatarajiwa kujihusisha zaidi katika maendeleo ya mnyororo wa thamani. Hii inajumuisha kukuza uwezo na ujuzi wao, kwa mfano, kwenye masuala ya masoko ya uuzaji mbao, kamati za maliasili zinahitaji mafunzo juu ya mchakato wa kutafuta wazabuni na namna mijadala ya makubaliano kwenye mikataba inavyofanyika, shughuli za uvunaji na usimamizi na pia katika uuzaji wa bidhaa za mbao pamoja na ufikiaji bora wa bei na taarifa zingine za soko.

Ili kuwezesha taasisi kupanga, kusimamia na kufuatilia usimamizi shirikishi wa misitu ya jamii na maendeleo ya mnyororo wa thamani, wadau wanahitaji kujengewa uwezo kuanzia ngazi ya vijiji, wilaya, mkoa na kitaifa. Katika kuendeleza maendeleo ya mnyororo wa thamani na faida zake kwa ajili ya usimamizi endelevu wa misitu ikihusisha masuala ya kijamii, kimazingira na namna ambavyo jamii na wadau wengine wanaweza kufaidika kwa kuongeza kipato na ajira, wadau watajengewa uwezo, ujuzi na uelewa katika dhana ya mnyororo wa thamani na adhari zake. Ukuzaji wa uwezo ni pamoja na kusaidia elimu ya ugani, huduma za mawasiliano na kuunganisha mafunzo ya mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu, mifumo ya masoko na maendeleo ya ujuzi wa biashara na mitaala katika taasisi za mafunzo.

Ukuzaji wa uwezo ni pamoja na kusaidia huduma za ugani na huduma za mawasiliano katika kuanzisha mifumo iliyoboreshwa ya ufuatiliaji. FORVAC inafanya kazi ili kuongeza usimamizi wa taarifa na mwamko wa umma juu ya utekelezaji wa Sera ya misitu. Kwa kuzingatia mpango wa ugani na huduma ya mawasiliano ulioandaliwa, utawezesha usambazaji wa taarifa ya Sera ya Misitu na maelekezo yanayohusu usimamizi shirikishi wa misitu na mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu. Majadiliano ya sera hufanyika pia katika ngazi ya kitaifa, kwa mfano Mikutano ya kitaifa ya misitu.

Katika usambazaji wa taarifa, msisitizo unawekwa katika kuingiza maswala ya usawa wa kijinsia na kuhakikisha upatikanaji wa taarifa kwa makundi tofauti, mfano kwa watu wasiojua kusoma na kuandika.

FORVAC imeanzisha Mfumo wa usimamizi wa taarifa (MIS) ili kupata usimamizi mzuri wa programu na kusaidia katika ukusanyaji na usambazaji wa taarifa kwa wadau. Mfumo huo utaunganishwa na mfumo wa taarifa za Idara ya Misitu na Ufugaji nyuki ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

FORVAC pia inachangia maboresho katika sera na mifumo ya kisheria ya ukuzaji wa thamani ya mazao ya misitu inayolenga kuoanisha mfumo wa kisheria na kisera ili kuongoza na kuboresha usimamizi endelevu wa misitu na biashara. Programu hii inasaidia Idara ya Misitu na Nyuki katika kuendeleza, kuboresha na kusambaza utaratibu na miongozo muhimu ya kiufundi ili kusaidia usimamizi wa misitu ya jamii. Kwa kuongezea, FORVAC inahakikisha uandaaji na marejesho ya sheria ndogo ndogo katika ngazi ya uwandani iendane na sera na sheria za kitaifa.

Maendeleo endelevu ya usimamizi wa sheria za misitu na nyuki yanajumuishwa kwenye majukumu ya Wizara ya Maliasili na Utalii (MNRT) na wakala wa huduma za misitu Tanzania (TFS). Serikali ya Tanzania pia inafanya kazi ya kuweka na kutekeleza sera ya Taifa ya Misitu na Nyuki na sera zingine, mfano kuhusiana na biashara. FORVAC inasaidia kuandaa sheria za misitu na sera zinazoelekeza majukumu ya jamii na ushiriki wa sekta binafsi katika misitu, sekta ndogo ya misitu na nyuki na biashara za ndani na nje ya nchi.