FORVAC KWA KIFUPI

Programu ya Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC) awali ilikuwa ni programu ya miaka 4 (Julai 2018 – Juni 2022) inaofadhiliwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland (MFA Finland) na kutekelezwa chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya Tanzania. Hata hivyo, mwezi wa Aprili 2022, serikali hizi mbili zilikubaliana kuendeleleza utekelezaji wa programu hii hadi Julai 2024. Inalenga kuongeza faida za kiuchumi, kijamii na kimazingira kutokana na usimamizi wa misitu kwa kuongeza thamani ya mazao ya misitu na kuimarisha maisha ya jamii kwa ujumla.

FORVAC ni muendelezo wa shughuli, uzoefu na masomo yaliyopatikana kutoka programu tatu zilizotekelezwa hapa nchini Tanzania na kufadhiliwa na Serikali ya Ufini: Programu ya Misitu na Ufugaji Nyuki wa Kitaifa (NFBKP II, 2013-2016), Uwezeshaji wa Kilimo Biashara katika mikoa ya Lindi na Mtwara (LIMAS, 2010–2016) na Programu ya Panda Miti Kibiashara (PFP, 2014–2019). Kama FORVAC inavyofanya, NFBKP II na LIMAS zilifanya kazi katika Usimamizi wa Misitu ya Jamii (CBFM) kwa kuendeleza usimamizi endelevu wa misitu na kutoa mapato na ajira kwa jamii katika Hifadhi za Misitu iliyotengwa. Programu ya Panda Miti kibiashara inatoa uzoefu katika maendeleo ya mnyororo wa thamani, uhamasishaji wa jamii za vijijini kwa shughuli za kiuchumi, na kuendeleza huduma za mafunzo ya ugani kwa wenye mashamba madogo ya misitu.